×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

TPDC YAENDELEA KUTEKELEZA MIRADI YA KIMKAKATI KUIMARISHA SEKTA YA MAFUTA NA GESI NCHINI

Na Mwandishi wetu.

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati inayolenga kuimarisha sekta ya mafuta na gesi asilia nchini, sambamba na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa Watanzania.

Akizungumza katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, Afisa Utumishi wa TPDC, Bw. Elinaike Nabuti, amesema kupitia ushiriki wake kwenye maonesho hayo, shirika hilo linaonesha kwa vitendo namna linavyotekeleza majukumu yake ya msingi, yakiwemo usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za mafuta na gesi kwa manufaa ya taifa.

“Elimu hii ni muhimu kwa wananchi ili waelewe fursa zilizopo katika sekta ya gesi na mafuta. Wanapata kujifunza kuhusu matumizi ya gesi asilia kwenye magari, majumbani, pamoja na miradi mikubwa kama ule wa LNG unaotarajiwa kutekelezwa mkoani Lindi,” amesema Nabuti.

Ametumia fursa hiyo kuwaalika wananchi kutembelea banda la TPDC ili kujifunza na kupata elimu zaidi kuhusu miradi mbalimbali inayotekelezwa na shirika hilo, ikiwemo matumizi ya gesi asilia kwa matumizi ya kila siku na mchango wake katika maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa TPDC, Bi. Marie Msellemu, amebainisha kuwa moja ya mafanikio makubwa ya shirika hilo ni usambazaji wa gesi asilia majumbani, ambapo kwa sasa huduma hiyo imewafikia wakazi wa mikoa minne ya Lindi, Mtwara, Pwani na Dar es Salaam.“

Tayari nyumba zaidi ya 5,000, magari takriban 7,000 pamoja na viwanda 57 vimeunganishwa na huduma ya gesi asilia. Hii ni hatua kubwa ya maendeleo katika kuhakikisha nishati safi inapatikana kwa matumizi ya kila siku,” amefafanua Msellemu.

Aidha, alieleza kuwa TPDC ina kituo kikubwa cha usambazaji wa gesi kilichopo Mlimani City, Dar es Salaam, ambacho kinahudumia vituo vingine vya kujaza gesi kwenye magari.

Hatua hiyo imechochea matumizi ya nishati safi, huku ikipunguza utegemezi wa nishati zenye madhara kwa mazingira kama vile mkaa na kuni.

#NTTupdates