×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

TUME YA UCHAGUZI YAHAKIKI MAOMBI YA UGAWAJI MAJIMBO HUKO MBAGALA.

Na Mwandishi wetu.

Mjumbe wa Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Balozi Omari Ramadhan Mapuri leo Aprili 23, 2025 ameongoza Kikao maalum kati ya Tume na Wadau wa Uchaguzi katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke lengo likiwa ni kujiridhisha Maombi yaliyowasilishwa ya kuligawa Jimbo la Mbagala ni sahihi na yalifata taratibu.

Akizungumza katika Kikao hicho Balozi Mapuri amesema”Kwa mujibu wa Kanuni ya 18 ya Kanuni za Tume huru ya Uchaguzi Mwaka 2024 Tume imechagua kutembelea baadhi ya Majimbo yaliyoomba kugawanywa kwa lengo la kujiridhisha iwapo taarifa zilizopo kwenye Maombi yaliyowasilishwa ni sahihi.

“Tulipokea Maombi ya mapendekezo ya kugawa Jimbo la Mbagala kupitia barua yenye Kumb.Na. CJA. 213/306 ya Tarehe 12/03/2025 kutoka kwa Katibu Tawala Mkoa hivyo lengo la kikao hiki ni kujiridhisha yaliyowasilishwa ikiwa ni sehemu ya jukumu la tume kushirikisha wadau wa uchaguzi”

Aidha Balozi Mapuri ameainisha Vigezo vya Ugawaji Majimbo kwa Mujibu wa ibara ya 75: 3,4 ambavyo ni idadi ya watu upatikanaji wa mawasiliano, hali ya kijiografia vilevile hali ya kiuchumi, ukubwa wa jimbo husika, mipaka ya kiutawala, Mpangilio wa Makazi ya watu yaliyopo, Mazingira ya Muungano n.k.

Akizungumza mara baada ya Wadau kuwasilisha maoni yao ya kuridhia kuwa ni sahihi maombi hayo yametoka kwa Wananchi na yamefata taratibu zote.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Albert Chalamila amesema”Usije ukatoka hapa ukasema Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi yaridhia Jimbo kugawanywa, kwa sasa Mchakato umeishia kupata Maoni yenu ninyi kama wamiliki wa wazo, alafu akitoka hapa atakwenda kukaa huko na jopo lote na kuendelea na michakato mingine inayohitajika kwa Mujibu wa Kanuni, Sheria na Taratibu alafu kama tunakidhi Vigezo wao ndio watakaotangaza kwamba sasa kuna Jimbo jipya lenye jina mlilopendekeza, lenye kata mlizopendekeza na kadhalika”

Kikao hicho kimehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wakiwemo Wenyeviti wa Vyama vya siasa, Wawakilishi wa Asasi za kiraia, Wazee, Wawakilishi wa Wananchi, Viongozi wa dini na Wataalam.

#NTTUpdates