Na Mwandishi wetu.
Mwenyekiti wa Umoja wa Maimam Tanzania (UMATA) Imam Suleiman Abdallah ametoa wito kwa watanzania wote kuendelea kuwa watulivu ili kudumisha amani tuliyonao katika taifa baada ya Uchaguzi.
mam Suleiman Abdallah ametoa wito huo akiwa jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kuwahamasisha watanzania kulinda tunu ya amani na utulivu mara baada ya kuwachagua viongozi wa Serikali za Mitaa Novemba 27, 2024.
Imam Abdallah amesema, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa umeshakamilika hivyo wananchi hawanabudi kuendelea kuwa watulivu ili kudumisha amani itakayotuwezesha kulijenga taifa na kumuabudu Mwenyezi Mungu ambaye ametutunuku amani tuliyonayo.
“Ili kuilinda amani tuliyonayo ni muhimu sana kwa wagombea walioshinda na kushindwa kuyapokea matokeo na wananchi pia wayapokee vizuri kwani demokrasia imechukua nafasi yake,” Imam Abdallah amesisitiza.
Katika kuhakikisha amani inalindwa, amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya taarifa potofu zinazohusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Novemba 27, 2024 ambazo zinasambazwa kupitia mitandao ya kijamii na baadhi ya watu wenye nia ovu ya kuleta taharuki na mifarakano ndani ya nchi ambayo imejaliwa amani na utulivu.
Aidha, Imam Adbdallah ameipongeza Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kwenye hatua zote za mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 27, 2024.
“Ninaipongeza TAMISEMI kwa kutoa elimu hususani kupitia SMS za kawaida, kitendo ambacho kimepelekea wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura ya kuwachagua viongozi wa Serikali za Mitaa,” Imam Abdallah amefafanua.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Novemba 27, 2024 umefanyika kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura 287 na Sheria Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura 288.
#NTTUpdates