Asema Tanzania inaingia kwenye historia nyingine ya kuwa mwenyeji wa Mkutano mkubwa wa Marais wa Afrika.
Na Mwandishi wetu.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila leo Januari 25, 2025 ameongoza mamia ya wananchi wa Wilaya ya Ilala kufanya usafi katika eneo la uwanja wa ndege wa Kimataifa Mwl JK Nyerere barabara ya Terminal One kuelekea mjini (City centre) ikiwa ni maandalizi ya mapokezi ya ugeni mkubwa wa Marais wa Afrika ambao wanatarajia kuwasili kuanzia leo.
Chalamila amesema Tanzania inaingia kwenye historia ya kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa wa Marais wa nchi za Afrika kujadili masuala ya Nishati ambao utafanyika tarehe 27-28/01/2025 katika ukumbi wa JNICC Jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo unakuja na fursa nyingi za kiuchumi kwa Mkoa na Taifa kwa ujumla ambapo Mhe Mkuu wa Mkoa amewataka wakazi wa Mkoa huo kuzitumia vizuri fursa hizo.
Aidha Chalamila amesisitiza umuhimu wa kuweka Mkoa katika hali ya usafi nyakati zote za ugeni huo ukiwa katika mkoa wetu na mara baada ya kuondoka tabia ya usafi iwe ni utamaduni wa kila siku kwa kila mtu.
Vilevile Chalamila amesema kwa kuwa ugeni huo ni mkubwa baadhi ya barabara zitafungwa kwa siku chache ambazo ugeni huo utakuwepo katika Mkoa wetu.
Mwisho Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe Edward Mpogolo ameshiriki pia katika zoezi hilo la kufanya usafi akiwa ameambatana na viongozi wengine wa Wilaya hiyo.
#NTTUpdates