×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

ULEGA AITAKA TEMESA KUJA NA TATHMINI CHANYA UJENZI WA VIVUKO VIPYA

Na Mwandishi wetu.

Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega ameutaka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), kufanya tathmini ili kujua athari chanya zitakazopatikana kwa jamii kutokana na ujenzi wa vivuko vipya sita vinavyoendelea kujengwa na kutarajiwa kukamilika hivi karibuni.

Akikagua ujenzi huo katika Karakana ya Songoro jijini Mwanza Waziri Ulega amesema Serikali kupitia TEMESA imetenga zaidi ya Shilingi Bilioni 56 kwa ajili ya ujenzi wa Vivuko vipya sita na ukarabati wa vivuko vingine vitano.

” Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka rekodi ya kutengeneza vivuko sita kwa wakati mmoja vitano katika Ziwa Victoria na kimoja Bahari ya Hindi hivyo ni muhimu kujua athari chanya kwenye uwekezaji huu muhimu”, amesema Waziri Ulega.

Amesema vivuko hivyo licha ya kuboresha huduma za usafiri na uchukuzi pia vitachochea ukuaji wa uchumi wa Kanda ya Ziwa na Taifa kwa ujumla.

“Toeni tathmini ya kiuchumi na kijamii, ni kitu kizuri na ni kitu muhimu sana maana kinahusisha watu, maisha yao na ule mchango wa kiuchumi na kijamii kwa mtu mmoja mmoja na taifa ndio tunataka tuufahamu”, amesisitiza Waziri Ulega.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu (TEMESA), Lazaro Kilahala, amevitaja vivuko vipya vinavyoendelea kujengwa na kutarajiwa kukamilika hivi karibuni kuwa ni Kivuko cha MV. UKEREWE kitakachotoa huduma kati ya Kisorya Wilayani Bunda Mkoani Mara na Rugezi Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza ambako kinakwenda kukiongezea nguvu kivuko MV. UJENZI ambacho kimeonekana kuzidiwa na wingi wa abiria wanaovuka kati ya maeneo hayo.

#NTTupdates