×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

VIONGOZI 35 WA NGAZI ZA JUU KUTUA TZ HAIJAWAHI KUTOKEA

Na Mwandishi wetu.

Idadi ya Wakuu wa Nchi watakaoshiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati uliopangwa kufanyika nchini Januari 27 na 28, 2025 ni rikodi nyingine kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema Wakuu wa Nchi 25 na Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu na Naibu Mawaziri Wakuu 10 inafanya idadi ya viongozi wa ngazi ya juu 35 ambao Tanzania tokea izaliwe haijawahi kupokea idadi kubwa ya viongozi kama hao katika tukio moja.

“Tulipokea Wakuu wa Nchi 19 wakati wa kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere mwaka 1999 na Wakuu wa Nchi 15 wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) mwaka 2019, mkiangalia idadi ya Wakuu wa Nchi katika mkutano huu ni kubwa ukilinganisha na matukio hayo mawili yaliyopita” Balozi Kombo alisema.

Alizitaja nchi ambazo Wakuu wa Nchi zao zimethibitisha kushiriki kuwa ni Pamoja na; Algeria, Comoro, Liberia, Lesotho, Botswana, Kenya, Ghana, Gabon, Sierra Leone, Ethiopia, Sudan, Malawi, Zambia, Somalia, Guine Bisau, Burundi, Mauritania, Kongo Brazzaville, Madagascar, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Libya, Nigeria, Djibouti na Gabon.

Makamu wa Rais watakaoshiriki ni kutoka Gambia na Benin. Mawaziri Wakuu kutoka Cote d’Ivoire, Uganda, São Tomé and Príncipe na Equatorial Guinea na Naibu Mawaziri Wakuu ni kutoka Eswatine na Namibia.Waziri Kombo amesema mkutano huo ni mwendelezo wa matunda ya diplomasia ya Tanzania ambapo Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kutangazika barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Amesema mwaliko wa Rais Samia Suluhu Hassan kushiriki katika Mkutano wa Nchi 20 Tajiri zaidi duniani (G20) uliofanyika Brazil Novemba 2024 na Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya Afrika na China (FOCAC) na kupewa na nafasi ya kuzungumza kwa niaba ya Bara la Afrika ni kielelezo cha diplomasia ya Tanzania kuimarika duniani.

#NTTUpdates