Na Mwandishi wetu.
Tume ya Madini imewataka wachimbaji wadogo wa madini kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni na miongozo ya usalama inayotolewa na wataalam wa sekta hiyo ili kukomesha ajali zinazoendelea kuripotiwa katika maeneo ya uchimbaji.
Wito huo umetolewa leo na Kamishna wa Tume ya Madini, Mhandisi Theonestina Mwasha, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya usalama kwa wachimbaji wadogo wa madini na wadau wa sekta ya madini kutoka mikoa ya Simiyu na Mara yaliyofanyika mjini Bariadi, mkoani Simiyu.
Mhandisi Mwasha amesema Serikali kupitia Wizara ya Madini imejipanga kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia elimu, vifaa na teknolojia ili kuwawezesha kujiinua kutoka katika uchimbaji wa kiwango cha chini hadi kuwa wachimbaji wa kati na baadaye wakubwa.
“Lengo kuu la mafunzo haya ni kuwaongezea uwezo wa kitaalam ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikumba sekta hii, hususan katika maeneo ya usalama migodini,” amesema Kamishna Mwasha.
Aidha, amewataka wachimbaji hao kuzingatia matumizi salama ya kemikali, hususan zebaki, kwa kuwa matumizi mabaya yake yamesababisha madhara yasiyorekebishika kwa afya ya binadamu na mazingira.
“Mafunzo haya yamejikita katika sheria na kanuni za usalama mahali pa kazi pamoja na Sheria ya Madini. Ni muhimu sana kuhakikisha mnafuata miongozo hii katika kutekeleza shughuli zenu,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mkaguzi Mkuu wa Migodi kutoka Tume ya Madini, Mhandisi Hamis Kamando, amesema ajali nyingi zinazotokea migodini husababishwa na kutokuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa na mamlaka husika.
#NTTUpdates