Na Mwandishi wetu.
Serikali kupitia Wizara ya Fedha imeendelea kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali katika Mkoa wa Mwanza, hatua inayolenga kuwawezesha kujenga misingi imara ya kifedha kwa maendeleo endelevu.
Wajasiriamali wa Kata ya Misungwi, Wilaya ya Misungwi, Mkoa wa Mwanza, wameelezea shukrani zao kwa Serikali kwa kuwawezesha kupata elimu ya fedha iliyotolewa na maafisa kutoka Wizara ya Fedha katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, yamewapa mwanga wa kupanga na kuimarisha ustawi wao wa kifedha.
Mafunzo hayo yamewalenga wajasiriamali, watumishi , wanafunzi, na wafugaji, yakiwa na dhima ya kuwawezesha kusimamia fedha zao kwa ufanisi, kuepuka mikopo umiza, na kujiandaa kifedha kwa maisha ya baadaye, ikiwemo kipindi cha kustaafu.
Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Misungwi, Afisa Sheria Bw. Steven Singila alisisitiza kuwa elimu ya fedha waliyoipata imewajengea uelewa wa umuhimu wa kujiwekea akiba, uwekezaji, na maandalizi ya maisha ya baadaye.
“Tunaomba pia tuendelee kupatiwa mafunzo ya ujasiriamali ili tuweze kuboresha miradi yetu na kujiandaa kwa maisha baada ya kustaafu. Kupitia elimu hii, tumejifunza kuwa hata kama kipato ni kidogo, bado kuna njia sahihi za kuweka akiba na kuwekeza kwa faida endelevu,” alisema Bw. Singila.
Aidha, Bi. Lucy Mbarika, kwa niaba ya washiriki wengine, alieleza kuwa elimu waliyoipata itawawezesha kufanya maamuzi sahihi ya kifedha, kuepuka madeni yasiyo na tija, na kutumia taasisi rasmi za kifedha kwa mikopo na uwekezaji.
“Mafunzo haya yametufungua macho kuhusu masuala ya kifedha, tumejifunza jinsi ya kupanga bajeti, kutenga akiba, na kuepuka madeni yasiyo ya lazima elimu hii itatusaidia sio tu kama wajasiriamali, bali pia kama familia na jamii kwa ujumla,” alisema Bi. Lucy.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu Mwandamizi wa Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro, alibainisha kuwa mwitikio wa wananchi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mwanza umekuwa wa kuridhisha.
“Tunaipongeza jamii kwa mwamko wao wa kutaka kujifunza na kutumia elimu ya fedha kwa ufanisi, tumejifunza kutoka kwa washiriki na maoni yao yatazingatiwa katika awamu zijazo za utoaji wa elimu ya fedha ili kuhakikisha inawafikia watu wengi zaidi,” alisema Bw. Kimaro.
Mafunzo ya elimu ya fedha ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha kuwa wananchi wanakuwa na uelewa sahihi wa masuala ya kifedha ili kuboresha maisha yao, kukuza uchumi wa kaya, na kupunguza utegemezi wa kifedha kupitia matumizi sahihi ya rasilimali walizonazo.
#NTTUpdates