
Zaidi ya watoto 200,000 wenye umri kati ya miaka 0 hadi 10 katika halmashauti ya Jiji la Mwanza wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya kuwakinga na ugonjwa wa polio ambao vimelea vyake vimetajwa kubainika katika mkoa wa Mwanza.
Akizungumza na wazazi katika kituo cha afya mkolani Jijini Mwanza, afisa Tawala wa halmashauri hiyo, Magreth John, ameeleza namnq ugonjwa huo unavyoweza kuhatarisha maisha ya mtoto iwapo hatopatiwa chanjo.
“nawahamasisha wazazi sana toeni ushirikiano kwa wataalam watakaopita katika maeneo yenu kutoa chanjo hiyo ili watoto wenu waweze kupata kinga”
Awali Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mwanza, Mfamasia wa Jiji la Mwanza Gipson simbulya ameeleza visababishi vya ugonjwa huo kuwa ni vimelea vinavyopatikana kwenye haja kubwa ambavyo vikisambaa vinaweza kusababisha madhara kwa watoto.

” Madhara anayoweza kupata mtoto mwenye vimelea vya polia ni kupooza miguu na wakati mwingine kusababisha kifo”
Aidha, amesema katika miaka ya nyuma waliweza kudhibiti ugonjwa huo lakini hivi karibuni walibaini uwepo wa vimelea hivyo jitihada za makusudi za kudhibiti ugonjwa huo zimeanza mara moja.
“Chanjo itatolewa kwa muda wa siku nne , tutapita mashuleni na nyumba kwa nyumba kuhakikisha watoto wote wanapatiwa chanjo, tuwaombe wazazi watoe ushirikiano ili kumkinga mtoto dhidi ya vimelea hivyo,” amesema
Hatahivyo diwani wa kata ya Mkolani John Mbira amesema wametoa elimu kuhakikisha wananchi wote wanatoa ushirikiano kwa wataalam watakaopita kwenye maeneo yao kutoa chanjo.

