×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

WATUMISHI WA LITA WAHIMIZWA KUZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA

Na Mwandishi wetu.

Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Mhina amewataka watumishi wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) kuzingatia Kanuni za Maadili ya Utumishi wa umma kwani taasisi yeyote ambayo haizingatii maadili ya Utumishi wa Umma ni vigumu sana kupata utendaji wenye tija.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe leo Aprili 04, 2025 Dodoma katika Kikao cha Utoaji Taarifa za Mkutano wa Kumi na mbili (12) wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA), Dkt. Mhina amesema kuna baadhi ya Watumishi wanashindwa kuzingatia Kanuni za maadili na Sheria za utumishi wa umma kutokana na uzembe na matokeo yake kuleta matokeo mabovu katika Taasisi.

“Tufanye kazi kwa bidii na kwa uaminifu kazini kwa kufuata misingi Mikuu ya Uadilifu, ikiwemo uwajibikaji na uaminifu,” amesema Dkt. Mhina.

Aidha, Dkt. Mhina amesema mtumishi anapaswa kutunza siri za ofisi kwa kutotumia taarifa za Serikali visivyo sahihi au bila idhini ya Utawala kwani Kanuni zinawataka kutunza taarifa kwa siri.

Vilevile, Dkt. Mhina ameitaka Menejimenti ya LITA kuwajengea watumishi wao uwezo na kuhakikisha wana utendaji mzuri kazi, na wanakuwa na uadilifu kwa kuzingatia Sheria na kanuni na Taratibu za Utumishi wa umma.Dkt. Mhina amewapongeza LITA kwa mpangilio mzuri wa kampasi ambao zimekuwa zinatoa fursa mbalimbali zinazoonekana kwa wafugaji.

Halikadhalika, Dkt. Mhina amesema bado kuna jukumu kubwa la kutoa mafunzo ya mifugo kwa wafugaji kwani chuo hakiwezi kuendelea kama hakiwekezi kwenye Miundombinu na ushirikishwaji wa jamii kwenye kutoa Mafunzo ya Mifugo.

Pia, Dkt. Mhina, ameipongeza Kamati ya Wajumbe wa Baraza Kuu LITA kwa kuendelea kujenga Vyuo vingine katika sehemu mbalimbali na amewataka Baraza kuisaidia Menejimenti katika kubuni Miradi mingine, ikiwa pamoja na kupima kama Mipango inaleta tija ambayo itaenda kufanya mabadiriko makubwa katika Taasisi baada ya miaka kadhaa ili kufanya maboresho makubwa zaidi.

Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA), Dkt. Pius Mwambene amesema wamepata nasaha kubwa kutoka kwa Mgeni Rasmi, na kuahidi kushirikishana katika Mipango yote ambayo imepangwa kwa Mwaka ujao wa fedha.

Dkt. Mwambene amesema wataendelea kuzingatia Maadili ya Utumishi wa Umma kwa kutekeleza Majukumu waliopewa na Serikali na kuwajibika ili kuleta matokeo chanya kwa Taasisi na nchi nzima.

#NTTupdates