×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

WAWILI MBARONI KWA TUHUMA ZA KUKUTWA NA NYARA ZA SERIKALI

Na Mwandishi wetu.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kupatikana na nyara za serikali bila kibali, huku mwingine akikamatwa na dawa za kulevya aina ya bangi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, amesema watuhumiwa hao wamekamatwa kwa ushirikiano kati yao na Askari wa Hifadhi ya Taifa (TANAPA), katika msako uliofanyika Mei 14, 2025 katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, wilayani Mbarali.

Miongoni mwa waliokamatwa ni Said Ngovano (30) mkazi wa Saadani – Mufindi, ambaye amekutwa akiwa na nyama za wanyamapori wa aina nne pundamilia, swala, ngiri na nyati.

Pia amekutwa na bunduki aina ya gobole, goroli mbili zinazotumika kama risasi, pamoja na kisu.

“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa ni muwindaji haramu. Atachukuliwa hatua za kisheria na kufikishwa mahakamani muda wowote kuanzia sasa,” amesema Kamanda Kuzaga.

Mtuhumiwa mwingine ni Marko Kweya (51) mkazi wa Kijiji cha Miyombweni wilayani Mbarali ambaye amekamatwa akiwa na meno manne ya tembo kilo 18 akiwa ameyaficha kwenye mifuko ya sandarusi wakati akiwa katika harakati za kuyauza.

Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi linamshikilia Hassan (40) mkazi wa Tanga, baada ya kukamatwa na dawa za kulevya aina ya bangi kilo 25, akisafiri kwa basi la abiria aina ya Yutong lenye namba za usajili T.809 DXJ la kampuni ya Abood, akitokea Mbeya kuelekea Dar es Salaam.

Amesema Hassan amenaswa kwenye kizuizi cha Polisi kilichopo eneo la Mpakani, wilayani Mbarali, akiwa ameficha dawa hizo kwenye sanduku.

Kutokana na matukio hayo, Kamanda Kuzaga ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kudhibiti ujangili na biashara haramu ya dawa za kulevya.

#NTTupdates