Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Daktari Jesca Lebba, amesema changamoto ya Watoto njiti kwasasa inasababishwa na ukosefu wa huduma maalum, uhaba wa vifaa tiba vya kisasa na uhaba wa wataalamu waliobobea katika afya ya Watoto wachanga.
Amesema jambo hilo linapelekea idadi kubwa ya Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati kupoteza maisha.
Daktari Lebba ametoa Kauli hiyo wakati akikagua ujenzi wa kitengo cha huduma Kwa Watoto wachanga (Neonatal Care Unit-NCU) katika wilaya ya Kwimba, Mkoani Mwanza.
Daktari Lebba amesema kuwa malengo ya Serikali ni kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa Wananchi na ujenzi wa kitengo hicho ni hatua muhimu ya kukabiliana na changamoto ya vifo vya Watoto njiti katika mkoa wa Mwanza na kuimarisha huduma ya Mama na Mtoto.
Mradi wa ujenzi wa kitengo hicho unajengwa kwa ushirikiano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Taasisi ya Doris Mollel Foundation kwa lengo la kutoa huduma bora kwa Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (Njiti) kama sehemu ya uboreshaji wa huduma ya Mama na Mtoto.