×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

RUKSA KUFANYA MALIPO KWA FEDHA ZA KIGENI

Na Mwandishi wetu.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa ufafanuzi kuhusu kanuni za matumizi ya fedha za kigeni za mwaka 2025, ikieleza kuwa malipo ya bidhaa na huduma kati ya wakazi na wageni wakiwemo watalii, yanaweza kufanyika kwa kutumia fedha za kigeni.

Akizungumza wakati wa mjadala uliofanyika kwenye maonesho ya Karibu-Kilifair Jijini Arusha, Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha wa BoT, Emmanuel Akaro amesema hatua hiyo inalenga kuwezesha mazingira rafiki ya kibiashara kwa wageni na urahisi wa miamala katika sekta ya utalii.

“Mawakala wa utalii ambao ni wakazi, wanaruhusiwa kutumia fedha za kigeni kulipia huduma mbalimbali zinazotolewa kwa watalii kutoka nje ya nchi,”ameeleza Akaro

Pia amesisitiza kuwa malipo yote kati ya wakazi lazima yafanyike kwa shilingi ya Tanzania, na ni kosa kwa mtoa huduma yeyote kukataa malipo yanayofanyika kwa kutumia shilingi.

Kanuni hizo zimetungwa kwa mujibu wa kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006, na zimeanza kutumika rasmi kuanzia Machi 28 mwaka huu.

#NTTupdates.