×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

SERIKALI YAZINDUA MAFUNZO YA KUONGEZA UJUZI WAKULIMA NA WASINDIKAJI WADOGO

Na Mwandishi wetu.

Serikali imezindua mafunzo ya kuongeza ujuzi kwa wakulima na wasindikaji wadogo katika sekta ya kilimo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uzalishaji, ubora wa bidhaa na kuinua kipato cha wananchi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Zuhura Yunusi, alisema serikali imepanga kutoa mafunzo hayo kwa wakulima na wazalishaji wadogo wapatao 1,000 katika mwaka huu wa fedha 2025/2026.

Zuhura amesema mafunzo hayo yatafanyika kwa ushirikiano na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), yakiwa na lengo la kuongeza ufanisi katika uzalishaji, kuimarisha njia bora za utendaji kazi, na kuboresha ubora wa mazao pamoja na bidhaa zinazotokana na kilimo.

“Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga Tanzania kuwa na uchumi shindani na wa viwanda, unaotegemea nguvukazi yenye maarifa na ujuzi. Mafunzo haya ni hatua muhimu kufikia lengo hilo,” amesema.

Ameongeza kuwa sekta ya kilimo bado ni mhimili wa uchumi wa taifa, ikichangia asilimia 26.5 ya Pato la Taifa, kuajiri takribani asilimia 65 ya nguvukazi, na kuzalisha asilimia 30 ya mapato ya mauzo ya nje.

Kwa mujibu wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2025–2030, serikali imepanga kuhakikisha mchango wa sekta ya kilimo katika pato la taifa unaongezeka kutoka asilimia 4.6 mwaka 2025 hadi kufikia asilimia 10 mwaka 2030.

“Serikali pia itaanzisha mfuko wa dhamana kupitia Mfuko wa Pembejeo za Kilimo, Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na Benki ya Ushirika, ili kuwawezesha wakulima kupata mikopo yenye riba nafuu,” amefafanua Zuhura.

#NTTupdates