Na Mwandishi wetu.
Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 14 wa Baraza la Usimamizi wa Mkataba wa Lusaka unaofahamika kama ( 14TH Governing Council Meeting of Parties to Lusaka Agreement) unaotarajiwa kufanyika kwanzia Mei 08, 2025 Jijini Arusha katika Hoteli ya Gran Melia.
Akizungumza na wanahabari Jijini Arusha hii leo Mei 07. 2025, Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Baraza la Usimamizi wa Mkataba wa Lusaka ulianzishwa mwaka 1994 kwa lengo la kuwezesha nchi za Afrika kusaidiana katika kukabiliana na ujangili na biashara haramu ya nyara ikiwemo biashara ya misitu inayovuka mipaka ya nchi bila ya kibali kutoka nchi husika.
Dkt. Chana amesema kuwa Tanzania ilijiunga na mkataba huo mwaka 1999 na imekuwa ikiutekeleza kwa kushirikiana na nchi wanachama ambayo ni Kenya, Lesotho, Congo- Brazzaville, Liberia na Zambia.
Aidha, amebainisha moja ya faida ya ushirikiano wa nchi hizo ni pamoja na kukabiliana na mitandao ya ujangili wa Wanyamapori na misitu, kufanya operesheni na doria na mafunzo ya kukabiliana na vitendo vya uhalifu.
Ikumbukwe kuwa mkutano huo hufanyika mara moja kila baada ya miaka miwili ambapo mara ya mwisho mkutano huo ulifanyika nchini Zambia mwezi Machi 2022.
#NTTupdates.