×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

TANZANIA YAJIPANGA KUONGOZA AFRIKA KATIKA MKUTANO WA COP30

Na Mwandishi wetu.

SERIKALI kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano, Mazingira imesema Tanzania imejipanga kuongoza Bara la Afrika katika Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP30), unaotarajiwa kufanyika kuanzia Novemba 10 hadi 21, 2025 jijini Belém, Brazil.

Akifungua kikao cha Makatibu Wakuu jijini Dodoma cha maandalizi ya ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian John Luhemeja, alisema Tanzania inatarajia kutumia nafasi yake kama Mwenyekiti wa African Group of Negotiators (AGN) kuibeba sauti ya pamoja ya Bara la Afrika katika mazungumzo hayo.

“Jukumu hili linaiweka Tanzania katika nafasi ya kipekee ya kuongoza majadiliano ya Bara zima, kuhakikisha vipaumbele vyetu vya pamoja vinapewa uzito unaostahili katika maamuzi ya kimataifa,” alisema Mhandisi Luhemeja.

Amebainisha kuwa mkutano wa COP30 utakuwa wa kihistoria kutokana na kufanyika kwake nchini Brazil moja ya waanzilishi wa Mkataba huo na kwamba utajikita katika kuchambua njia za haraka za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi baada ya zaidi ya miaka 30 ya utekelezaji wake.

Mhandisi Luhemeja amesema vipaumbele vya Tanzania katika mkutano huo vinaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, iliyozinduliwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan Julai 17, 2025, ambayo inalenga kujenga taifa lenye ustawi, jumuishi na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi.

Mshauri wa Rais katika masuala ya mazingira na Mwenyekiti wa Kundi la Afrika la Majadiliano, Dkt. Richard Muyungi, ameeleza kuhusu ajenda kuu ambayo Bara la Afrika linaibeba kuelekea kwenye mkutano huo.

Nae Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, Mhandisi Ussi Khamis Debe akimwakilisha Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar anaelezea lengo la kikao hicho.

#NTTupdates