Na mwandishi wetu
WANANCHI wamepewa wito wa kushiriki katika wiki ya Kitaifa ya Ufuatiliaji na Tathmini itakayofanyika Jijini Arusha ambayo itahusisha kutoa elimu itakayowawezesha kutoa taarifa za Ufuatiliaji na Tathmini na Ufuatiliaji wa Miradi mbali mbali ya kimaendeleo inayofanywa na Serikali katika maeneo yao.
Hayo yameelezwa leo Tarehe 28 Agosti 2023, na Mtakwimu Mkuu kutoka Idara ya Ufuatliaji na Tathmini ya Ofisi Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Thomas Saguda, alipokuwa akizungumza na Kituo kimoja cha Televisheni Jijini Dodoma.
Bwn. Saguda Alisema, Wananchi hao wanaweza kushirki kupitia maonesho mbalimbali yatakayoonesha kazi mbalimbali za Ufuatiliaji na Tathmini zilizofanyika ndani ya nchi na kupata kujionea mengine yatayooneshwa na washiriki mbalimbali kutoka nje ya nchi.
“Maonesho haya yatawapa fursa wananchi ya kuelewa namna wanavyopaswa kufanya Ufuatiliajia na Tathmini, wenzetu wataalam wanaita Citizen Science, ni rahisi sana Mwananchi ukimuuliza mradi flani wa maji pale umefanya kazi, atakwambia unafanya kazi, ama atakwambia maji pale yalitoka wiki mbili tuu yakakatika, kwa hiyo yule anakupa taarifa ya uhakika, kwa sababu ndiyo mnufaika na ndiyo mlengwa.” Alisema bwana Saguda.
Aliendelea kusema kuwa Sambamba na Maonesho hayo Kongamano hilo pia litahusisha mafunzo ya kitaaluma, warsha mbalimbali zitakazoendeshwa na wataalamu wabobezi wa masuala ya Ufuatiliajia na Tathmini kutoka ndani na nje ya nchi na kuongeza kusema kuwa mada mbali mbali zimekwisha wasilishwa kwa ajili ya Utekelezaji.
Awali akiongea katika kipindi hicho maalum, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. JohnBosco Quman, alisema Eneo la Ufuatiliaji na Tathmini linamgusa kila mmoja, aliyepo Serikalini au katika Sekta Binafsi kwani Utekelezaji wa Miradi mingi inatekelezeka katika jamii na inamgusa kila mmoja, “Ukiangalia katika ngazi ya Wizara Sera ndo zinatekelezeka huko, lakini kwenye suala la utekelezaji linashuka kwenye ngazi ya Halmashauri na ndiko kwenye wadau mbalimbali, kwa hivyo kwa kupitia miradi kama vile ya Afya na Maji, Serikali inavyotoa fedha na kusimamia miradi hiyo, matokeo yake yanamgusa kila mmoja.” Alibainisha Bw. Quman
Aliendelea Kufafanua kuwa Idara hii ina jumuku kubwa la kuhakikisha kuwa kile ambacho kinachotolewa na Serikali kinaenda kunufaisha jamii nzima.
Sambamba na hilo, Kongamano hili la Pili la Kitaifa la Wiki ya Ufuatiliaji na Tathmini litakalofanyika Jijini Arusha mapema mwezi Septemba, itawalenga zaidi,wataalam wa Ufuatiliaji na Tathmini, Maafisa na Mameneja wa Miradi kutoka katika Taasisi zote za Umma, Taasisi Binafsi, makampuni, Asasi za Kiraia na mashirika ya Kimataifa.
#NttUpdates