
Wajumbe wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Kilimanjaro, wakiongozwa na mwenyekiti wao, wamefanya ziara katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa lengo la kujifunza na kujionea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Miradi iliyotembelewa na ALAT Kilimanjaro ni pamoja na shule ya mchepuo wa Kiingereza (Nyanza English Medium) inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana, pamoja na kujifunza mbinu za kisasa za ukusanyaji wa mapato zinazotumiwa na halmashauri hiyo.
Akizungumza baada ya kuhitimisha ziara hiyo katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saa Nane, Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Kilimanjaro, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Rombo, Gilbert Tarimo, amesema ziara hiyo imekuwa na mafanikio makubwa na kuwawezesha kujifunza mambo mbalimbali, ikiwemo ukusanyaji wa mapato kwa mfumo wa kisasa na uanzishaji wa miradi ya maendeleo.
“Nichukue fursa hii kuwakaribisha wenzetu wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza waje kujifunza kwetu Kilimanjaro ili tuweze kubadilishana uzoefu wa kiuongozi. Pia, wanapopata nafasi, waje kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii, ikiwemo Mlima Kilimanjaro,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Moshi, ambaye pia ni Katibu wa ALAT Mkoa wa Kilimanjaro, Shadrack Mhagama, amesema wameona umuhimu wa kujifunza kutoka katika halmashauri nyingine zinazotekeleza kwa ufanisi majukumu ya kuwahudumia wananchi.
Ameongeza kuwa lengo kuu la ziara hiyo ni kujifunza mbinu mbalimbali za kukabiliana na changamoto pamoja na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.
Aidha, amebainisha kuwa wamejifunza namna halmashauri zinavyotekeleza miradi ya maendeleo kulingana na fedha zinazotolewa na Rais wa Awamu ya Sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na utoaji wa huduma kwa wananchi katika sekta za elimu na afya.
“Katika Jiji la Mwanza, tumeona mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali. Tumejionea shule ya mchepuo wa Kiingereza inayotoa huduma kwa gharama nafuu, na wananchi wamehamasika kupeleka watoto wao katika shule hiyo.
“Pia tumetembelea Hospitali ya Wilaya, ambapo tumejionea ujenzi wa majengo mbalimbali ukiendelea, hususan yale yaliyopata ufadhili wa serikali, pamoja na utoaji wa huduma bora za afya. Hakika tumejifunza mengi,”
