MKURUGENZI Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph ameleza mkakati wa kupeleka maji katika mji wa Kibaigwa kwa kuchimba visima ili kukabiliana upungufu wa maji.
Mhandisi Aron alioa maelezo hayo baada ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo kumtaka kujibu mbele ya wananchi namna ya kuondokana na kero ya upungufu wa maji.
Alisema DUWASA ambayo imekabidhwa kuhudumia mji huo Juni 9 mwaka huu inatoa maji kwa mgao kutokana na uzalishaji kuwa mdogo ikilinganishwa na mahitaji.
Alisema mahitaji ya maji ni lita milioni 3.7 kwa siku na uwezo wa kuzalisha ni lita milioni 2.3 na hivyo kuwa na upungufu wa lita milioni 1.4 kwa siku.
“Hata hizo lita miloni 2.3 hatuzizalishi inavyotakiwa kutokana na changamoto ya umeme na tumekuwa tukizalisha kwa saa 10 hadi saa 12, hivyo wananchi hawa wanaweza kupata maji mara mbili ya wanavyopata sasa kama tutakuwa na umeme wa uhakika.”
Mhandisi Aron alisema baada ya kukabidhiwa kutoa huduma, DUWASA imetembelea chanzo cha maji na kubaini kumilikiwa na wananchi hivyo kuhitaji ulipaji fidia ili wananchi waachie bonde hilo.