×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

NAIBU WAZIRI AITAKA JAMII KUVUNJA UKIMYA VITENDO VYA UKATILI.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mwanaidi Ali Khamis ameitaka jamii kutokukaa kimya na kunyamazia vitendo vya ukatili vinavyotokea ili kuwa na Jamii iliyo salama hasa kwa Wanawake na Watoto.

Ameyasema hayo wakati wa ziara yake mkoani Geita Septemba 11, 2023 iliyolenga kufuatilia utekelezaji wa sera na mipango mbalimbali ya wizara katika Mamlaka ya Mikoa na Serikali za Mitaa nchini.

“Nimefika katika Mkoa huu wa Geita nimepokea taarifa ya Mkoa nimeona masuala ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto yameshamiri, jumla ya mashauri 625 kwa watu wazima na mashauri 133 ya vitendo dhidi ya watoto yameripotiwa, sasa tusikae kimya tupaze sauti tutokomeze ukatili.” Amesema Mhe. Naibu Waziri.

Aidha amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii kuwasikiliza wananchi katika maeneo yao ili kuwasaidia kutatua changamoto mbalimbali wanazokabilia nazo katika jamii hasa za upatikitanaji wa fursa za kiuchumi na ukatili wa kijinsia.

“Ndugu zangu Maafisa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii Rais Samia Suluhu Hassan ameiunda Wizara hii muhimu mtusaidie kuwafikia wananchi kutatua changamoto zao, tuwasaidie wananchi tuwasikilize.” Amesisitiza Naibu Waziri.

Wakati huo huo Naibu Waziri Mwanaidi amepokea taarifa ya Utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) katika Kata ya Nyamigota na amewasihi wajumbe wa kamati ya MTAKUWWA kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii ili wawe na uwezo wa kutoa taarifa za vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kuilinda jamii.

Pia Naibu Waziri Mwanaidi ametembelea Kikundi cha Manyuki Company Grading Rice killichopo Mamlaka ya Mji mdogo wa Katoro Halmashauri ya Wilaya ya Geita na kuwataka Wanawake kujiunga katika vikundi vya kiuchumi ili waweze kupata fursa mbalimbali za kupata mikopo kwaajili ya kupata mitaji na masoko ya bidhaa wanazozalisha katika vikundi vyao.

Kwa upande Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Geita Karia Rajab Magaro amemuhakikishia Naibu Waziri Mwanaidi kuratibu masuala yote ya Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii na kuhakikisha Maafisa wa kada hizo wanawafikia wananchi kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika jamii.

“Nakuhakikishia Mhe. Naibu Waziri, tutayasimamamia masuala yote ya Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita ili wananchi waweze kupata huduma na namna za kupambana na changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii yetu,” amesema Magaro.

NttUpdates