×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

TANROADS DAR ES SALAAM YAWASHIKA MKONO WENYE UHITAJI

Na Mwandishi wetu.

WATUMISHI wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam, wametoa msaada wa mahitaji muhimu ya kibinadamu katika kituo cha Furaha na Amani cha Mtakatifu Thereza cha Mburahati jijini Dar es Salaam.

Akiongoza watumishi hao Meneja wa Mkoa huo, Mhandisi John Mkumbo amesema, mahitaji hayo ya vitu mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni mbili na elfu thelasini (2,030,000) yamewasilishwa ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma inayofanyika kila mwaka nchini.

“Tunashukuru umetutembelea kila mahali wanapoishi watoto wa umri mbalimbali, wazee wasiojiweza na watoto wenye changamoto ya kimwili, tumejionea mazingira yalivyo na hata uhitaji ninaamini kuna siku Mungu atatuongoza tutakuja tena kutoa mahitaji yanayostahili,” amesema Mkumbo.

Naye Mhasibu Mwandamizi wa TANROADS Dar es Salaam, Bi. Neema Mtengula amesema mbali na kuwa ni wajenzi wa barabara ili zipitike vizuri lakini pia wamekuwa wakitoa misaada kwa jamii zenye uhitaji katika vituo vya kulea wazee na watoto.

Kwa upande wake Sista, M. Gonzalo M,C amewashukuru wafanyakazi hao wa TANROADS kwa majitoleo yao kwa ajili ya kituo hicho, amewaomba wasiwachoke na wafike mara kwa mara kuwasaidia maana bado wanauhitaji wa vitu mbalimbali kwa ajili ya watoto na wazee wanaolelewa hapo.

Sista amesema kuwa wanawapata watoto wa kuanzia umri wa sifuri hadi miaka mitatu kutoka kwenye ofisi za Ustawi wa jamii wakiwa wengine wametelekezwa na wazazi wao hawajulikani, na wengine wanachangamoto za ulemavu wa viungo.

“Ninashukuru sana kwa moyo wenu mkuu mmeweza kutembelea nyumba yetu ya wahitaji mmejionea wenyewe wapo watoto wadogo sana jumla tuna watoto 34, wazee wasiojiweza 42 na watoto wenye changamoto mbalimbali za viungo wapo 22 bado tunahitaji misaada kutoka sehemu mbalimbali maana tuna watoto wadogo sana na wazee wengi hawajiwezi,” amesisitiza Sista Gonzalo.

#NTTUpdates