*Ahimiza ushirikiano wa kikanda kuchochea ukuaji wa uchumi
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewahimiza viongozi na watendaji wa Serikali kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha usalama wa kikanda ili kuchochea uwekezaji wa kikanda na kimataifa.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Aprili 16, 2026) mkoani Kigoma wakati akifungua Kongamano la Biashara na Uwekezaji la Ziwa Tanganyika (The Lake Tanganyika Business and Investment Forum) linalofanyika kwa siku nne katika ukumbi wa Hoteli ya Lake Tanganyika, mjini Kigoma.
Kongamano hilo ambalo lilianza jana (Jumatano, Aprili 15, 2026) linawakutanisha viongozi wa Serikali, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchi zinazozunguka Ziwa Tanganyika zikiwemo Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Tanzania ambayo ni mwenyeji wa kongamano hilo.

Akizungumzia kongamano hilo, Waziri Mkuu amesema makongamano ya aina hiyo yana mchango mkubwa katika kuimarisha ushirikiano miongoni mwa mataifa yanayoshiriki. “Tuna imani kuwa kongamano hili litaibua matumaini mapya ya ushirikiano wa Ukanda wa Ziwa Tanganyika,” amesema Waziri Mkuu.
“Ukanda huu ndiyo unaongoza kwa madini adimu duniani, na dunia ipo kwenye mwelekeo wa matumizi ya madini haya, hivyo sisi ni matajiri wa madini hayo na hatuna budi kuimarisha ushirikiano ili madini hayo yawanufaishe wananchi. Hivyo ni muhimu kushirikiana kuimarisha na usalama wa ukanda huu; na makongamano kama haya yanachangia pakubwa kuboresha ushirikiano huo kwenye nyanja zote,” amesema.
Waziri Mkuu amesisitiza kuwa mkoa wa Kigoma una fursa na rasilimali nyingi ambazo bado hazijatumika ikiwemo ardhi kubwa yenye rutuba, vivutio vya utalii, madini na viwanda vinavyotoa nafasi ya kuchochea uwekezaji mkoani humo.

“Kigoma siyo mkoa wa pembezoni kama ilivyokuwa imezoeleka zamani, bali ni mkoa wa katikati unaounganisha biashara, uwekezaji na uchukuzi katika ukanda wa Ziwa Tanganyika. Kigoma ni mwanzo wa reli kuelekea nchi za jirani na mwanzo wa reli kuelekea ukanda wa kati wa nchi yetu, hivyo ni mkoa muhimu kwa uwekezaji nchini na kwa mataifa ya jirani,” amesisitiza.
Dkt. Mwigulu amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji ikiwemo kuwa na nishati ya uhakika na miundombinu ya usafiri na uchukuzi inayokidhi mahitaji. Pia, amewataka viongozi na watendaji wa Serikali waweke mikakati ya kuimarisha usalama ili kuchochea uwekezaji wa kikanda na wa kimataifa.

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema kongamano hilo ni jukwaa muhimu la kuyaunganisha kiuchumi mataifa yanayozunguka Ziwa Tanganyika ambapo miradi mingi ya kimkakati katika sekta ya uchukuzi inatekelezwa ili kuendelea kuufungua ukanda huo.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro amewahakikishia wafanyabiashara na wawekezaji kuwa Kigoma ipo salama, kwani uhalifu uliokuwa ukifanyika miaka ya nyuma umedhibitiwa na sasa Kigoma ni sehemu salama kwa uwekezaji.
Amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuufanya mkoa wa Kigoma kuwa kitovu cha biashara kwa nchi zinazozunguka Ziwa Tanganyika kutokana na miradi mingi ya kimkakati inayowekezwa hivi sasa mkoani humo na hivyo kuufungua mkoa huo na kuufanya kuwa lango muhimu kwa nchi za ukanda wa Ziwa Tanganyika.
Naye, Gavana wa Jimbo la Tanganyika la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Christian Kifungwa Muteba ameishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana na nchi hiyo katika nyanja mbalimbali ikiwemo ulinzi na usalama.
Amesema kuwa uwekezaji wa bandari kubwa katika Ziwa Tanganyika utarahisisha usafirishaji wa madini adimu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwenda nchi nyingine bila kulazimika kupitia katika mataifa yaliyo mbali na nchi hiyo.
Mapema, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Dkt. Latifah Khamis alisema kongamano hilo limewakutanisha wadau mbalimbali ili kujadili na kutatua changamoto za kibiashara na uwekezaji kati ya nchi shiriki ambazo ni za Ukanda wa Ziwa Tanganyika.
Alisema wadau hao wanajumuisha viongozi na watendaji wa taasisi za umma na binafsi pamoja na wafanyabiashara 256 ambapo 63 kati yao wanatoka nje ya nchi.


