
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, ametoa rai kwa watumishi wa umma kutumia kwa uangalifu magari mapya yaliyotolewa na serikali, akisisitiza kuwa ni mali ya walipa kodi na yanapaswa kutunzwa ili yaweze kudumu na kutoa huduma iliyokusudiwa.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa hafla ya kukabidhi vitendea kazi kwa Mahakama ya Tanzania pamoja na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Waziri Homera amesema matumizi mabaya ya magari hayo yanaweza kuisababishia serikali hasara na kuwanyima wananchi huduma bora.
“Rai yangu ni kuwa magari haya tuyatunze, watu wasije wakaendesha kwa fujo na kesho tukasikia gari limepata matatizo. Hatuwezi kujisikia vizuri, tutahuzunika kwa sababu haya ni mali ya serikali na fedha za walipa kodi,” amesema.
Ameeleza kuwa wizara ina imani kubwa na taasisi hizo kutokana na kazi nzuri wanazozifanya, jambo lililosababisha kuchukua jukumu la kununua magari ya kisasa pamoja na vifaa vingine muhimu ili kuboresha utendaji kazi.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema serikali imeendelea kuzipatia taasisi mbalimbali vitendea kazi, ikiwemo kompyuta zaidi ya 50 zilizokabidhiwa kwa Mahakama ya Tanzania, hatua ambayo amesema itachochea mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma za haki.




