×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

MAAFISA MAZINGIRA MWANZA WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA NEMC KUDHIBITI UCHAFUZI

Maafisa mazingira Mkoani Mwanza wametakiwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ili kupata miongozo sahihi ya usimamizi wa mazingira, huku wananchi wakihimizwa kufuata na kusimamia utekelezaji wa Sheria Namba 191 ya mwaka 2004 iliyoboreshwa mwaka 2023, kwani wanao wajibu wa kutunza mazingira.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda na huku akisema kuwa Mkoa wa mwanza unakumbwa na changamoto mbalimbali za kimazingira, ikiwemo uchafuzi wa Ziwa Victoria, ongezeko la takataka za plastiki, athari za uchimbaji wa madini, na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na shughuli za kibinadamu.

Mtanda, ameleza kuwa wananchi, na wadau wa serikali, na wadau mbalimbali kushirikiana katika kudhibiti uchafuzi wa mazingira, huku akisisitiza kuwa changamoto kubwa ya uchafuzi inahitaji hatua za pamoja kutoka kwa pande zote za kijamii, kiuchumi, na kisiasa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Usimamizi wa Sheria ya Mazingira kutoka NEMC, Bw. Elibariki Bajuta, amesisitiza kuwa NEMC inaendelea kushirikiana na viongozi wa Mkoa wa Mwanza katika kutoa elimu kwa wananchi na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria.

Kwa upande mwingine, Bi. Sylvia Autophace, mtaalamu wa masuala ya kimazingira kutoka kampuni ya Nyanza Road Works Ltd, amesema ni muhimu kwa wataalamu wa mazingira kutoa ushauri sahihi kwa wawekezaji ili kuhakikisha kuwa miradi ya madini inafanyika kwa kuzingatia mazingira.

Mwanasheria kutoka Ziwa Steel and Wire Products Ltd, Philipo Sylivanus, ameeleza changamoto zinazozikumba sekta ya uwekezaji katika usajili wa miradi na usimamizi wa vibali vya mazingira.

Sylivanus ameongeza kuwa wadau wengi wanapokuwa wanasajili miradi, mara nyingi wamekuwa wakiacha jukumu la usajili kwa wataalamu wa mazingira (environmental experts), lakini wao kama wenye miradi hawafuatilii maendeleo ya mchakato huo kwa karibu.

NTTUPDATES.